Sunday, March 5, 2017

Maoni ya Shaffih Dauda kuhusu Pluijm kusitishiwa mkataba na Yanga


Baada ya klabu ya Yanga kusitisha mkataba wake na aliyekuwa mkurugenzi wao wa ufundi Hans van der Pluijm ambaue pia aliwahi kuwa kocha mkuu wa kikosi hicho kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na George Lwandamina, kumekuwa na mitazamo tofauti kuhusu Hans kusitishiwa mkataba ndani ya ‘wakimataifa’.
Shaffih Dauda mchambuzi wa michezo kutoka Clouds Media Group naye pia ametoa maoni yake huku akiunga mkono uamuzi wa Yanga kusitisha mkataba na Hans kutokana na hali mbaya ya kiuchumi wanayopitia kwa sasa.
Dauda hakubeza uwezo na mafanikio ya Hans ndani ya kikosi cha Yanga lakini amesema kutokana na mifumo ya soka la Tanzania, Yanga kuendelea kubaki na Hans ni kujipa gharama kubwa ambazo si za lazima ikilinganishwa na kazi anayoifanya ndani ya Yanga kwa sasa.
“Ni maamuzi sahihi kwa Yanga kuamua kusitisha mkataba wa Hans kwa sababu tayari wana benchi la ufundi,” – Shaffih Dauda.
“Baada ya Hans kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa ufundi wa Yanga, niliwasifu viongozi wa klabu hiyo kwa sababu kilikuwa ni cheo kipya, nikawa naona Yanga wanaelekea pazuri. Kwa sababu majukumu ya mkurugenzi wa ufundi ni mapana zidi sit u kujikita na kikosi cha kwanza lakini ana majukumu ya kutengeneza mifumo ya timu kupitia timu za vijana.”
“Yanga waliona umuhimu wa soka la vijana na kuamua kuelekeza nguvu zao huko, lakini kwa mazingira ya soka la kibongo walikuwa wanamlipa Hans mshahara wa bure kwa nafasi yake na majukumu aliyopewa kuyatekeleza.”
“Hans alifanikiwa kwa kiasi kikubwa wakati akiwa kama kocha mkuu wa Yanga, moja ya mafanikio yake makubwa zaidi ni kuifikisha Yanga kwenye hatua ya makundi ya kombe la shirikisho Afrika baada ya Yanga kusota kwa muda mrefu bila kufika hatua hiyo kwenye michuano yote ya Afrika.”
“Lakini pia amefanikiwa kuchukua ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara pamoja na Azam Sports Federation Cup (FA Cup) pamoja na kuijenga Yanga kuwa kikosi kipana na chenye ushindani ndani na nje ya Tanzania kutokana na kufanya usajili ambao mara nyingi umeisaidia timu.”
“Msingi wa kikosi cha Yanga hadi leo ni kutokana na usajili uliofanywa na Hans, Lwandamina bado hajafanya usajili wa wachezaji wengi labda kutokana na muda aliofika ulikuwa ni wa dirisha dogo. Lwandamina aliongeza wachezaji wawili tu, Justine Zulu na Emanuel Martin.”
“Amekuwa ni kocha kwenye mafanikio kwenye mechi za Simba na Yanga, kwa sababu ukiwa kocha wa vilabu vya Simba na Yanga mbali na kupata matokeo mazuri lakini bado mashabiki wanataka kocha apate matokeo chanya wanapokutana na watani wao wa jadi.”
Nimepewa taarifa leo (jana) asubuhi kwamba mkataba wangu umesitishwa kutokana na hali mbaya ya kiuchumi ndani ya klabu. Nawashukuru mashabiki kwa kunipa ushirikiano na kuniunga mkono kwa kipindi chote nilichokuwepo Yanga.

No comments:

Post a Comment